Al-Iman Society of Northamptonshire

Login   |    Signup  |

Utangulizi

Mfuko wa misiba ni mchango ulioanzishwa na Jumuiya ya Al Iman ya Northamptonshire ili kusaidia gharama za mazishi kwa watakaofariki au kufiwa na jamaa zao ambao wanaishi nao na kuwahudumia. Hii ni kwasababu ya kutokuwa na uwezo wa kujigharamia wao wenyewe ikiwa kwa ujumla au baadhi ya gharama hizo.

 

Mfuko ulianza rasmi Januari 2004.

 

Jumuiya ya waislamu wanaozungumza lugha ya Kiswahili na wakaazi wa Northamptonshire - Al Iman - wameona umuhimu wa kuanzisha mfuko huu kutokana na ukubwa wa gharama za mazishi hapa Uingereza ambazo kila siku huwa zinaongezeka na kuweza kujikuta wafiwa kupatwa na mshtuko baada yakuondokewa na jamaa zao na wakati huo huo kuingizwa katika deni zito ambalo kila siku kuweza kuongezeka kwa njia ya riba ikiwa halitopata mtu wa kulilipia.

 

Katika sheria ya kiislamu, endapo muislamu atafariki, waislamu waliopo watapaswa kuhakikisha kwama maiti anafanyiwa mambo mane ya kimsingi: Kuoshwa, kukafiniwa, kusaliwa na kuzikwa kwa mujibu wa taratibu za dini. Inabaki kuwa ni Fardhu ‘Ayn (wajibu wa lazima) mpaka kikundi cha waislamu watakapoyatekeleza na hapo huwa Fardhu Kifayah (ya kutoshelezana- ambapo wakifanya baadhi ya waislamu ,huporomoka hukumu kwa wengine). Kisheria, gharama za mazishi zinatakiwa kutolewa kwenye mali ya marehemu na hubaki kuwa deni mpaka lilipwe kwa niaba yake.

 

Michango hii itakuwa ikihudumia na kusaidia waislamu wanaozungumza Kiswahili na wakaazi wa jimbo hili pamoja na wachangiaji katika maeneo mengine yaliyojiunga kwenye mfuko endapo watatokewa na faradhi na hawakuwa na uwezo.

 

Kila akataejiunga na mfuko na kuchangia atakuwa anatoa sadaka ambayo itaweza kumsaidia yeye mwenyewe au wanaomtegemea na pia kuweza kusaidia waislamu wengine wasiokuwa na uwezo wanapofikwa na fardhi tukitekeleza agizo lake Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam kwamba “Mwenye kumpunguzia muislamu mwenzake mzigo katika mizigo ya kidunia basi Allah atampunguzia mzigo katika mizigo ya siku ya kiama”

 

Katika hali ya dharura tu ambapo aliyefariki au mfiwa hana uwezo wa kulipia gharama hizi, Idara ya huduma za jamii (Department of Social Services) inaweza kusaidia baada ya kuhakikisha hakuna wa kuzisimamia gharama hizi miongoni mwa jamaa wa marehemu au mfiwa kutokuwa na akiba iliyopo Benki au sehemu nyengine inayoweza kusimamia mazishi yake.

 

Uingereza kuna mifuko tofauti ambayo husimamia suala zima la mazishi kama pensheni, bima ya maisha na gharama zinazolipiwa kabla (pre paid funeral fund). Hata hivyo mfuko huu ni tofauti na mifuko hii kwani unaendeshwa kwa kufuata misingi na taratibu za kiislamu, hauhusiani na riba na kuhudumia wanaochangia na wasiokuwa na uwezo wa kuchangia ikiwa hawatokuwa na uwezo wa kujilipia gharama hizi. Pia mfuko unatambulika na Charity Commission hapa kwamba moja katika malengo yake ni kutoa msaada kwa wasiokuwa na uwezo wakati wanapofiwa na jamaa zao.

 

Mfuko unafanya kazi kwa wahusika kujitolea - fii sabiili llah – kwa ajili ya Allah Subhaanahu Wata’ala na bila ya malipo ya aina yoyote na upo chini ya Al –Iman ambayo ni jumuiya ya kujitolea kama ilivyosajiliwa Charity Commission.